Search
Free School Management System
Free School Management System for Kenya

Free School Management System

Learn More

2015 KCSE Murang'a South Mock

Kiswahili Paper 2

1.UFAHAMU (Alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yafuatayo.
1.

Vitabu vingi vya hadithi za watoto vilivyowahi kuandikwa katika lugha ya Kiswahili kufikia sasa vinaweza tu kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa darasa la nne hadi la nane na hivyo basi kuacha ombwe pale panapostahili kuwekewa msingi imara - shule ya chekechea hadi darasa la tatu. utafiti uliowahi kufanywa na wanaisimu-saikolojia unathibitisha kwamba uwezo wa mwanafunzi wa kujifunza lugha ya pili huwa katika kiwango cha juu awapo na umri mdogo na kwamba uwezo huo huanza kupungua kadiri umri unavyoongezeka na kufikia kipindi maalum (critical period) ambacho hukisiwa kubisha katika umri wa kubaleghe au kuvunja ungo.

Hivyo basi, ili kustawisha hulka ya usomaji ya kudumu, waandishi wa fasihi ya watoto wanapaswa kujifahamisha mengi kuhusu ukuaji wa watoto hao wadogo na mikakati ambayo huitumia katika kujifunza lugha ya pili.

Aidha, wanapaswa kuyafahamu yale yanayowapendeza na kuwachochea katika kusoma ili kuyajumuisha katika vitabu vyao vya hadithi. Mambo haya yatatimia iwapo waandishi hao watakuwa na mafunzo ya kimsingi katika taaluma ya isimusaikolojia.

Wanafunzi katika viwango tofauti wana mikakati tofauti ya kujifunza lugha ya Kiswahili. Kufikiria kwamba wanafunzi wa madarasa ya chini (darasa la kwanza, pili na tatu) wanaweza kuitumia mikakati sawa na ile ambayo hutumiwa na wenzao wa madarasa ya juu kujifunza Kiswahili si sahihi.
Watoto wadogo hujifunza mambo mengi kwa kukariri, kuigiza, kuiga, kufuatilia hadithi kwa picha miongoni mwa mbinu nyingine. Ili kufanikiwa katika kuwaandikia, sharti mikakati hiyo ya ujifunzaji izingatiwe.

Ufundi mkubwa unahitajika si tu katika kuziunda sentensi zao bali pia katika kuifinyanga sarufi. Sentensi zenyewe ziwe fupi, zenye sarufi na msamiati sahili, zilizorudiwarudiwa ili kuzifanya zinate akilini na kuendelezwa kwa mtindo wa nyombo au mashairi mepesi.

Watoto wadogo huvutiwa sana na nyimbo na mashairi mepesi na hujifunza kwa urahisi kupitia kwayo. Msururu wa vitabu vya ‘Someni kwa Furaha’ uliotumiwa katika miaka ya themanini na mwanzomwanzo wa miaka ya tisini ni mfano wa vitabu vilivyotekeleza dhima muhimu sana katika kuumua na kuchochea hamu ya wanafunzi kupenda kukisoma Kiswahili.

Vitabu hivyo vilitumia mbinu mbalimbali zilizoweza kuyateka mawazo ya wanafunzi katika viwango tofauti.

Miongoni mwa mbinu hizo ni matumizi ya vibonzo, mashairi na nyimbo za chekechea zenye maudhui ambayo watoto wangeweza kujinasibisha nayo. Baadhi ya nyimbo hizo zilihimiza umuhimu wa kusomea katika mazingira safi, ushirikiano katika shughuli mbalimbali na umuhimu wa kuyachangamkia masomo. Mfano mzuri ni huu wimbo unaopatikana katika kimojawapo cha vitabu katika msururu huo: Chawa chawa mchafu, petu ni pakavu Kata nyika utosini, kata nywele kwa mashine Kichwa safi kama nini? Chawa chawa mchafu, petu ni pakavu.

Mbinu nyingine iliyotumiwa sana katika vitabu hivyo ni matumizi ya picha na vibonzo. Vitabu vya watoto vinapaswa kuwa na picha nyingi au vibonzo vingi kuliko maandishi. Picha na vibonzo vyenyewe viwe vya rangi kwa sababu watoto huvutiwa sana na rangi.

Waandishi wa fasihi ya watoto katika Kiingereza wamefanikiwa pakubwa katika kukumbatia mbinu hii na hivyo basi kuyakidhi mahitaji ya rika tulilolitaja kwa kuandika vitabu ambavyo vimechangia kwa akali kubwa katika kustawisha hulka ya usomaji kuanzia shule ya chekechea hadi darasa la nane. Hali hii ni tofauti na Kiswahili ambapo hulka ya usomaji bado ingali changamoto kubwa kwani huanza kuwekewa msingi katika darasa la nne.

Kiini hasa cha kuendelea kuwepo kwa mielekeo hasi na matokeo mabaya katika somo la Kiswahili ni kule kukosekana kwa vitabu faafu vya hadithi za watoto katika madarasa ya chini vinavyoweza kusaidia katika kujenga hulka ya usomaji mapema iwezekanavyo.

Ombwe hilo linaweza kufidiwa tu iwapo waandishi wataibuka na vitabu ambavyo vitayakidhi mahitaji ya watoto
hao wadogo na kuwapa ari ya kukipenda Kiswahili kuanzia umri wa chini.
Maswali.
1. Kipe kifungu anwani mwafaka. (alama 1)
2. Ni katika umri gani mwanafunzi hujifunza lugha ya pilikwa kwa urahisi? (alama 1)
3. Waandishi wa vitabu vya watoto watastawisha usomaji wa kudumu kwa njia gani? (alama 4)
4. Taja dhana potovu kuhusiana na ujifunzaji lugha kwa watoto. (alama 2)
5. Onyesha njia ambazo kwazo watoto hujifunza kwa wepesi. (alama 3)
6. Vitabu vya watoto vinapendekezwa viwe na sifa gani? (alama 2)
7. Eleza maana ya msamiati huu kulingana na muktadha wa matumizi. (alama 2)
(a) Ombwe
(b) Kufidiwa

15 marks

2.UFUPISHO (Alama 15)

2.

Watu wengine hawawezi kunywa chai au uji bila kutia sukari. Wanatumia sukari kwa hamu na ghamu bila kutambua kuwa hiyo ni sumu wanayojiongezea mwilini.

Ni ukweli usiopingika kuwa wazee wa jadi waliishi muda mrefu wakiwa na siha njema kuliko sisi. Hii ni kwa kuwa waliishi katika kipindi ambacho sukari inayotengenezwa viwandani haikuweko. Iwapo ilikuweko, ilikuwa bidhaa ya wateule waungwana kutengenezea vitu kama keki, mahamri, vitumbua na kadhalika na akina yakhe hawangeweza kuigharamia.

Watafiti wa masuala ya afya wamegundua kuwa sukari inayotayarishwa viwandani sasa haina virutubishi vyovyote. Halikadhalika, utaratibu wa viwandani wa kutayarisha sukari ili iwe nyeupe na kuichuja huharibu virutubishi vinavyoweza kuwa muhimu mwilini. Umuhimu wa sukari wakausaza kwa kutia ladha tamu tu.

Umuhimu huu hauwezi kulinganishwa na madhara yanayoletwa na sukari hii. Baada ya kusagika mwilini, sukari hii huacha masalio ya asidi mwilini yenye sumu inayoathiri siha.

Matumizi ya sukari kwa wingi husababisha madhara mbalimbali mwilini. Kwanza, huchangia kuoza na kuharibika kwa meno pamoja na matatizo ya meno kuuma. Pili, sukari nyeupe imehusiwa na ongezeko la madhara ya kisukari, moyo na hipoglisimia au upungufu wa sukari mwilini. Matumizi holela ya sukari huleta kipandauso au ugonjwa wa gahfla wa kuumwa upande mmoja wa kichwa unaoambatana na kichefuchefu, kutapika na matatizo ya kuona. Pia sukari huleta maradhi ya ngozi na figo, pamoja na ongezeko la kemikali iitwayo kolestroli, ambayo ni ufuta unaonata na ambao unatokana na kutoyeyuka kwa mafuta yote mwilini. Kemikali hii ya kolestroli inaporundikana moyoni, hufanya mishipa inayotoa damu moyoni na kuisambaza mwilini kuwa myembamba na sugu. Moyo hulazimika kusukuma damu kwa nguvu na huenda moyo ukachoka na kukoma kufanya kazi.

Madhara haya ya sukari ndiyo yanayowafanya watu wengi kukiri kuwa sukari, ingawa ni tamu, ni sumu mwilini. Wataalamu wa lishe wamependekeza ulaji wa vyakula kama nafaka, matunda, mboga na miwa ambavyo vimejaa sukari asilia. Fauka ya hayo, sukari inayotoka katika asali ni bora zaidi kwa mwili wa mwanadamu. Asali huwa na sukari asilia, vitamini, madini na amino asidi. Hivi vyote huwa na manufaa mbalimbali mwilini.

Mathalani, asali huupa mwili nishati inayohitajika kuendesha shughuli za viungo. Licha ya hayo, asali
huuchangamsha mwili. Asali huwa na kemikali ambazo husaidia watoto kukua vizuri. Huweza kuzidisha kiwango cha himoglobini, hivyo kupunguza uwezekano wa watoto kuwa na anemia (upungufu wa damu). Halikadhalika asali husaidia katika usagaji wa chakula iwapo itatumiwa kabla ya mlo. Matumizi ya kijiko kimoja cha asali kila siku husaidia mwili kujikinga dhidi ya magonjwa ya kukohoa. Asali husaidia pia kuondoa harufu mbaya kinywani.

Asali pia inaweza kutumiwa kujipaka. Inapotumiwa kwa njia hii, hutunza ngozi na kuifanya ing’are huondoa vipele na ugumu wa ngozi, pamoja na kutibu kule ngozi ilikokatikakatika. Halikadhalika, asali hutibu vidonda.

Viwanda vingi vya vipodozi vilevile hutumia asali kama malighafi muhimu katika utengenezaji wa bidhaa hizo.

(a) Kwa kurejelea aya ya tatu na ya nne, dondoa mawazo yote muhimu.
(Tumia maneno 90) (al 7, 1 Utiririko)
(b) Fupisha aya ya tano na sita kwa kutumia maneno 70. (al 6, 1 Utiririko)

15 marks

3. MATUMIZI YA LUGHA. (Alama 40)

3.

Yakinisha sentensi hii.
Yeye siye asiyejua kwetu.

2 marks

4.

Tenga mofimu katika neno hili.
Watembeavyo.

2 marks

5.

Eleza maana ya sentensi ambatano kisha utolee mfano.

2 marks

6.

Andika neno lenye sauti moja ya koromeo.

1 marks

7.

Andika kinyume cha sentensi hii.

Aliamba kwamba wizi ulikuwa umepungua.

1 marks

8.

Onyesha maana mbili za neno mlango.

1 marks

9.

Tumia kiambishi ndi- pamoja na nomino ya ngeli ya KI-VI wingi katika sentensi..

2 marks

10.

Badilisha kivumishi kilichoko katika sentensi kwa kivumishi cha kusisitiza.

Mtoto msichana amechelewa shuleni tena.

1 marks

11.

Changanua kwa njia ya mstari.
Rinda na mamake walimchukua mtoto aliyekuwa ametoroshwa.

1 marks

12.

Kiima ni nini?

2 marks

13.

Nyambua katika kauli ya kutendewa.

Dada analia chumbani.

2 marks

14.

Onyesha matumizi ya viambishi viwili vya mahali katika sentensi moja.

2 marks

15.

Andika sentensi hii katika wingi.
Jaribio la shambulizi lilizimwa na askari.

2 marks

16.

Fuata maagizo.
(i) Tunamwombea (ifanye kishazi tegemezi)
(ii) Shiba (ifanye nomino)

2 marks

17.

Ainisha nomino katika sentensi hii;
Jopo lilitarajiwa kusema ukweli.

2 marks

18.

Tumia ki ya masharti kuandika upya sentensi hii;
Atakuja kisha tuende kwao.

2 marks

19.

Andika upya katika wakati uliopita hali timilifu.
Wanamaliza wali.

2 marks

20.

Unganisha ili kuonyesha hali ya kuamrisha.
Wewe + Sije

2 marks

21.

Andika katika msemo halisi.
Alfa alimwomba asimpeleke kwa mwalimu mkuu. Naye angempa zawadi. Akataka kujua kama anakubali.

2 marks

22.

Eleza aina ya kielezi kilichopigwa mstari.
Kadzo alipambana kiume.

2 marks

23.

Sahihisha bila kuondoa ‘enye’.
Gari lenye lilitujia halikuwa na utingo.

2 marks

4.ISIMU JAMII (Alama 10)

24.

Kiswahili ni mojawapo ya lugha za kibantu. Thibitisha kauli hii.

10 marks

Back Top